Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Kamati Kuu ya Kufufua Urithi katika Atabatu Abbasiyya imefanya kikao cha maandalizi kwa kushirikiana na Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Kufa, kwa lengo la kujadili vipengele vya utafiti vya mkutano wa tatu wa kimataifa wa kitaaluma wa maandalizi ya kuadhimisha miaka elfu moja ya Hawza tukufu ya Najaf.
Kikao hicho kiliandaliwa na Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Sheikh Tusi, kilicho chini ya kamati hiyo, kwa ushirikiano na Jumuiya ya Kitaaluma na Kifikra ya Al-Ameed, Chuo Kikuu cha Al-Kafeel na Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Kufa.
Mkutano huo utafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Hawza tukufu ya Najaf: Miaka elfu moja ya mchango usiokoma”, na utajadili mada isemayo: “Urithi wa kifasihi na kilugha wa Hawza tukufu ya Najaf katika karne ya 13 na 14 Hijria.”
Mkutano huo umepangwa kufanyika tarehe 16 na 17 Desemba 2026 Miladia, sawa na tarehe 6 na 7 Rajab 1448 Hijria, ambazo zinakubaliana na tarehe 25 na 26 Azar 1405 katika kalenda ya Hijria Shamsia.
Sheikh Muslim al-Ridhai, mshauri wa kamati hiyo, alisema kuwa kikao hicho kilifanyika katika makao makuu ya kamati na kililenga kujadili vipengele vya utafiti na kitaaluma vya mkutano huo. Aidha, kilijadili utaratibu wa kupitia na kutathmini makala za kitaaluma kupitia kamati maalumu za kielimu, ili kuhakikisha kwamba urithi wa kudumu wa kifasihi na kilugha wa Hawza tukufu ya Najaf katika karne ya 13 na 14 Hijria unafanyiwa uchunguzi na kuzingatiwa kwa umakini unaostahili.
Kikao hicho ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya kitaaluma inayoandaliwa na kamati hiyo kwa ajili ya kuadhimisha miaka elfu moja tangu kuanzishwa kwa Hawza ya Najaf. Shughuli hizo zinalenga kuangazia mafanikio ya Hawza katika nyanja za elimu na maarifa, kuonesha mchango wa wanazuoni wake wakubwa katika fani mbalimbali za elimu, pamoja na kuweka kumbukumbu na kuhifadhi urithi wake na kubainisha athari zake katika maendeleo ya ustaarabu wa binadamu kwa kipindi cha karne nyingi.
Maoni yako